MMOJA AFARIKI, WAWILI WAJERUHIWA WAKIBISHANIA SIMBA NA YANGA

 











Na Mwandishi Wetu, Mwanza. 

MTU mmoja amefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya kutokea ugomvi uliozuka kutokana na ushabiki wa mpira kati ya mashabiki wa timu za Simba na Yanga Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Kwa mujibu taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa amesema tayari wameanzisha msako wa kumtafuta kijana mmoja (jina limehifadhiwa) kwa tuhuma za kumuua Abel Mganga Mazuri (25) mkazi wa Nyamahengo, na kuwajeruhi watu wawili kufuatia ugomvi uliotokana na ushabiki wa mpira.

Taarifa hiyo imesema tukio hilo limetokea Machi 24, 2026 majira ya saa 5:30 usiku katika kitongoji cha Nyamahengo, kijiji na kata ya Sumve, wilayani Kwimba, mkoani Mwanza.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeanza msako wa kumtafuta kijana mmoja (jina limehifadhiwa kwa sasa) kwa tuhuma za mauaji ya Abel Mganga Mazuri, miaka25, mkazi wa Nyamahengo aliyeuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani kisha kuwajeruhi watu wawili kwa kutumia kitu chenye ncha kali wakati wanakunywa pombe na kuangalia mpira kwenye banda la maonesho ya mpira, katika kata ya Sumve, wilayani Kwimba,"

Taarifa hiyo ya Kamanda Mutafungwa imesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha shambulio hilo ni ushabiki wa mpira uliovuka mipaka na kuleta ubishani mkali kati ya mashabiki wa klabu za Simba na Yanga. 

"Waathirika wote wamepatiwa fomu za matibabu ya polisi (PF3) na hivi sasa wanapata matibabu katika Hospitali Teule ya Sumve ambapo hali zao zinaendelea kuimarika. Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kumtia mbaroni mtuhumiwa ili afikishwe katika vyombo vya sheria. "





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.