MHUBIRI WA KIMATAIFA DKT DANA MOREY AWASHA MOTO WA INJILI TABORA
Na Allan Kitwe, Tabora.
WAKAZI wa Manispaa ya Tabora na Mikoa jirani wamemiminika kwenye mkutano mkubwa wa injili unaohubiriwa na Mwinjilisti wa Kimataifa kutoka nchini Marekani Dkt Dana Morey ulioanza jana Mjini Tabora na kupokea baraka na uponyaji.
Wakizungumza baada ya kuombewa na Mwinjilisti huyo wameeleza kufurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Mkoa kuruhusu mkutano huo uendelee baada ya awali kuuzuia kwa kile kilichoelezwa kuwa wanagwa vitu visivyo na maadili kwa jamii.
Mkazi wa kata ya Tambuka-Reli katika Manispaa hiyo Magreth Lutaha (60) amweleza kuwa alikuwa na tatizo la uoni hafifu kwa zaidi ya miaka 10 lakini baada ya kuombewa na Mwinjili huyo amepokea uponyaji na sasa anaona vizuri.
‘Namshukuru Mungu nilikuwa sioni vitu vya mbali na kichwa kilikuwa kinaniuma kwa muda mrefu sana ila baada ya maombi kichwa hakiumi tena na sasa naona hata vitu vya mbali’, amesema.
Mariam Mayani (40) mkazi wa Nzega na Furaha Jungu (30) mkazi wa Kiloleni katika manispaa ya Tabora wameeleza furaha yao baada ya kuponywa mapepo, maumivu ya kifua na mgongo yaliyowatesa kwa zaidi ya miaka 5.
Naye Agness Lukumay (34) mjasiriamali mkazi wa Wilaya ya Sikonge ameeleza kuwa alikuwa na tatizo la mgongo lililomtesa kwa zaidi ya miaka 3 na hata akishika mimba zilikuwa zinatoka, lakini baada ya kuombewa maumivu yameisha.
Akihubiri mkutano huo katika uwanja wa shule ya msingi Kanyenye katika siku ya kwanza Mwinjilisti Dkt Dana amesema kuwa Yesu Kristu ndiye mponyaji, na yeyote atakaye sikia neno na kuliamini atapokea uponyaji wa mwili na roho.
‘Nimewaletea habari njema za Yesu Kristu mwana wa Mungu aliye hai, aliyetolewa kwa ajili ya wanadamu wote, ambaye ana uweza na mamlaka ya kuponya magonjwa yote na walio tasa kupata mimba kwa uweza wake’, amesema.
Awali akifungua mkutano huo Mwakilishi wa Makanisa ya Kipentekoste, Askofu na Mkurugenzi wa Kituo cha Runinga cha Agape cha Jijini Dar es salaam Dkt Venon Fernandes ameeleza kuwa Mwinjilisti Dana ni Mtumishi wa Mungu aliyejishusha na Mungu anamtumia kwa namna ya kipekee sana.





Maoni