FDC URAMBO WAJIVUNIA MAFANIKIO MAKUBWA
Na Allan Kitwe, Urambo.
CHUO Cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Urambo kimeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu na kukipatia vifaa vya mafunzo ambavyo vimekiongezea mapato.
Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Chuo hicho Elias Niima alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake ambapo alieleza kufurahishwa na uamuzi wa serikali ya Awamu ya Sita kukifanyia maboresho makubwa chuo hicho.
Amesema kuwa kipindi cha miaka 4 ya Uongozi wa Rais Samia na siku 100 za awamu yake ya pili tangu aingie madarakani, chuo kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kuzalisha samani za taasisi mbalimbali na kuingiza mapato.
Ametaja baadhi ya samani zilizotengenezwa kuwa ni madawati, viti na meza zaidi ya 7,000 kwa shule za msingi na sekondari za halmashauri za Wilaya ya Urambo na 2,500 za halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.
‘Miradi hii imetekelezwa na Chuo kwa kutumia nguvu kazi ya wanafunzi na walimu wao, ikiwa ni sehemu ya mazoezi yao kwa vitendo, hili limepelekea wanafunzi wa fani husika kupata uzoefu wa kutosha na kifuta jacho pia’, amesema.
Aidha chuo kilipewa fursa ya kutengeneza samani za milango 400 na fremu 400 za madarasa na mabweni ya shule Maalumu ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa ya Dkt Batilda Burian iliyojengwa mwaka jana Wilayani Kaliua.
Aidha milango zaidi ya 300 na fremu za milango 300 ya shule mpya za sekondari katika Wilaya ya Urambo zilitengenezwa hivyo kuwezesha chuo kujipatia mapato ambayo yamekuwa kichocheo cha kutatua changamoto za watumishi.
Niima ametaja mafanikio mengine kuwa ni kutoa mafunzo ya kozi fupi kwa vijana wa kike na kiume (wanagenzi 75) walioletwa na serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, mradi huo ulikiingizia Chuo zaidi ya shilingi milioni 33.
Kozi zilizofundishwa kwa wanagenzi hao ni ushonaji, ufundi umeme na upishi, kozi zilizoongezwa baadaye ni uungaji vyuma, ufundi magari, uashi na uselemala, wahitimu hao sasa wameajiriwa na wachache wamejiajiri.
Miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na chuo hicho hadi sasa ni ufugaji nyuki unaofadhiliwa na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) wenye thamani ya shilingi milioni 30 na ule wa nishati safi ya kupikia wa kuhifadhi mazingira.




Maoni