BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA TANGANYIKA YABORESHA VYANZO VYA MAJI

 


Na Allan Kitwe, Kigoma. 

BODI ya Maji ya Bonde laZiwa Tanganyika imefanikiwa kuboresha uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji vilivyopo katika Mikoa 8 na Halmashauri 28 za Miji, Manispaa na Wilaya zilizopo katika Ukanda wa Magharibi mwa Tanzania.

Hayo yamebainishwa juzi na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika Bona Mremi alipokuwa akiongea na wanahabari Ofisini kwake Mkoani Kigoma.

Amefafanua shughuli zilizofanywa na Bodi hiyo katika Kanda hiyo kuwa ni kulinda, kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji ikiwemo mabwawa, mito, chemichemi, maziwa, maeneo oevu na fukwe za bahari.

Shughuli nyingine ni kufuatilia mwenendo wa maji katika vyanzo vyote na kugawa maji kwa matumizi mbalimbali, kuongeza idadi ya Jumuiya za Watumiaji Maji kutoka 8 hadi 12 na kupanda miti zaidi ya milioni 2 katika vyanzo vya maji.

‘Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizotuwezesha kutekeleza majukumu yetu ya kusimamia, kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji kikamilifu’, ameeleza.

Aidha aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wadau kushiriki kikamilifu katika usimamizi na uendelezaji rasilimali za maji katika maeneo mbalimbali.

Kaimu Mkurugenzi amedokeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Bodi ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo na shughuli za kiofisi ikiwemo uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Amebainisha kuwa ndani ya siku 100 tangu Rais Dkt Samia aingie madarakani katika awamu yake ya pili, Bodi inajivunia kupata mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza Jumuiya za Watumiaji Maji kutoka 8 hadi 12 za sasa.

Jumuiya hizo ni Churumwama, Mkama, Nyamagoma, Sagara Juu-Kaliua katika kidakio cha Ugalla na Malagarasi katika Wilaya za Kaliua Mkoani Tabora na Uvinza Mkoani Kigoma.

Mafanikio mengine ni kuongeza tafiti za maji chini ya ardhi kutoka 59 hadi 71, kukagua vituo vya kukusanyia takwimu za kihaidrolojia, kutenga bajeti ya kukarabati mabwawa 4 na kukabidhiwa seti 3 za mitambo ya kuchimba visima.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.