WAZIRI AWESO APELEKA NEEMA URAMBO
Na Allan Kitwe, Tabora.
WAKAZI wa Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora wamelipuka kwa shangwe na furaha baada ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso kuagiza maji ya ziwa Victoria yafikishwe katika Wilaya hiyo ndani ya wiki tatu kuanzia sasa.
Waziri ametoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na mamia ya wakazi wa Wilaya hiyo katika Kata ya Muungano baada ya kutembelea na kukagua Mradi wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa na serikali ya awamu ya sita katika Wilaya tatu za Mkoa huo.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 143 ili kuleta maji ya uhakika ya ziwa Viktoria katika Wilaya za Kaliua, Urambo na Sikonge ambazo zinashida kubwa ya maji.
‘Mradi huu utekelezaji wake unaenda vizuri sana, ujenzi wa tanki kubwa la kupokelea maji tayari umekamilika, na nimeambiwa kuwa kipande kilichobakia hakizidi hata kilometa moja maji yatakuwa yamefika hapa Urambo’, ameeleza.
‘Nitawaongezea shilingi milioni 500 za mabomba ili kazi hii ifanyike haraka zaidi na maji yafike katika hili tanki ndani ya wiki tatu na kazi ya kuyasambaza kwa wananchi ianze mara moja’, amedokeza.
Aidha ili kuhakikisha wakazi wa Wilaya hiyo wanapata maji safi na salama ya uhakika aliahidi pia kuongeza kiasi cha shilingi milioni 400 ili RUWASA waweze kukamilisha haraka ujenzi wa mradi wa Bwawa la Maji la Kalemela.
Amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Mwajuma Waziri kuhakikisha fedha hizo zinaletwa haraka iwezekanavyo ili miradi hiyo miwili ikamilike kwa wakati na wananchi waanze kunufaika na serikali yao.
Wakitoa neno la shukrani, Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Hamis Mkanachi na Mbunge wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta wamempongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwaletea mradi huo na Waziri Awesu kusimamia ipasavyo utekelezaji wake.
Wamebainisha kuwa furaha na shangwe ya wananchi itakamilika pale watakapoona maji hayo yamefika katika nyumba zao na kuanza kuyanywa, ili kumaliza kero yao, hivyo wakaomba Waziri ambane Mkandarasi ili aharakishe kazi hiyo.




Maoni