WANANCHI WATAKIWA KUZINGATIA MIPANGO YA MATUMIZI BORA YA ARDHI
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WANANCHI wametakiwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kukidhi mahitaji ya sasa na baadaye katika shughuli za kilimo, ufugaji na makazi ili kuendelea kulinda na kuhifadhi maeneo yakiyohifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), katika kikao cha 7 cha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la Mhe. Onesmo Merdson Mnkondya (Mb), aliyehoji kuhusu mpango wa Serikali kuwapa kipande cha ardhi Wananchi wanaozunguka Hifadhi ndogo ya Isalalo iliyo chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Mhe. Chande amefafanua kuwa hifadhi ya msitu Isalalo ilianzishwa kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji, mimea na wanyama, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi udongo kwa kuwa msitu huo unazungukwa na jamii ya vijiji vitano ikiwemo Itentula na Hamwelo, Nambizo, Ipapa, na Utambalila ambavyo ni muhimu katika kulinda mazingira.
“Serikali kwa sasa haina mpango wa kumega hifadhi hiyo kwa matumizi ya kibinadamu. Hivyo, Serikali inawaruhusu wananchi kuendesha shughuli ambazo hazikinzani na uhifadhi ndani ya hifadhi kama vile ufugaji nyuki ambao baadhi ya wanachi tayari wameanza kufanya shughuli hizo katika hifadhi hiyo.” Amefafanua Mhe. Chande.




Maoni