VIGOGO WAWILI CCM WAFARIKI DUNIA

 L




Na Allan Kitwe, Tabora

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Mshauri wa Chama na Kiongozi katika nafasi mbalimbali za chama na serikali Mzee Nassoro Hamdan (84) amefariki dunia jana jijini DSM.

Aidha aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Tabora kwa miaka 20, Bi.Munde Abadllah Tambwe naye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.  

Akizungumzia misiba hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Saidi Nkumba ameeleza kusikitishwa na taarifa hizo na kubainisha kuwa wameondokewa na watu muhimu sana kwa chama na jamii kwa ujumla.

Ameeleza kuwa Mzee Hamdani ambaye ni Mwanzilishi wa Kampuni ya Mabasi ya NBS Classic Ltd ya Mjini Tabora na Munde walikuwa nguzo muhimu sana kwa Chama kwa jinsi walivyokuwa wakijitoa, hakika chama kimepata pigo kubwa.

Ameongeza kuwa Mzee Hamdan ambaye alijulikana zaidi kwa jina la NBS ametumikia chama hicho tangu akiwa kijana mdogo na aliendelea hivyo hadi ukubwani akitumika katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Baadhi ya nafasi alizowahi kushika ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Mlezi na Mashauri wa Chama, Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora, Diwani wa Kata ya Gongoni na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa.

Nyingine ni Mlezi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete na Mlezi wa Shule ya Watoto Wasioona ya Furaha iliyopo katika manispaa hiyo, pia alikuwa mdau mkubwa wa shughuli za maendeleo katika Mkoa huo.

‘Mzee Hamdan alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha shughuli za chama zote zinafanikiwa na alijitoa sana kwa wana Tabora wote pasipo kujali itikadi za vyama vyama wala dini, hakika tutamkumbuka sana Mzee wetu’, amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Upendo Wella ameeleza kuwa wamepokea misiba hiyo kwa masikitiko makubwa kwa kuwa viongozi hao walikuwa wadau muhimu sana, walitoa fedha zao nyingi kusaidia shughuli za maendeleo.

Katibu wa CCM wa Mkoa huo Wilson Nkambaku ameeleza kuwa marehemu walikuwa nguzo muhimu sana kwa maendeleo ya chama na jamii kwa ujumla, amedokeza kuwa mazuri waliyoyafanya yatakumbukwa daima na wanaCCM wote.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.