UWT TABORA WAMLILIA MUNDE TAMBWE

 


Na Allan Kitwe, Tabora.

UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoani Tabora wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa huo kupitia Jumuiya hiyo Bi.Munde Tambwe aliyefariki dunia juzi jijini DSM.

Akizungumza na gazeti hili jana Katibu wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Tabora Rhoda Madaha ameeleza kuwa marehemu alikuwa nguzo muhimu sana kwa maendeleo ya wanawake wote wa Mkoa huo.

‘Marehemu alikuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanawake na Vijana wa Wilaya zote za Mkoa wetu kuanzisha miradi ya kiuchumi ili kujikwamua kimaisha na alikuwa anatenga bajeti yake kuwawezesha’, ameeleza.

Madaha amebainisha kuwa enzi za uhai wake, marehemu alikuwa karibu zaidi na wanawake na kila akirudi kutoka bungeni alikuwa na agenda moja tu ya kukutana na makundi mbalimbali ya akinamama na kusikiliza kero zao.

Ameongeza kuwa ukarimu na ukaribu wake kwa wanawake ulimpa kibali sana ndio maana amekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa awamu nne za miaka mitano mitano na katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana aligombea Jimbo la Sikonge.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini Mohamed Katete ameeleza kuwa marehemu Tambwe alikuwa Kiongozi hodari na mchapa kazi, aliyependwa sana na wananchi na alitumia rasilimali zake kuwainua kiichumi.  

‘Marehemu alikuwa mfano wa kuigwa, alikipenda sana Chama Cha Mapinduzi, alijitolea sana kwa mambo mengi ili kuhakikisha shughuli za chama zinatekelezwa  kama zilizopangwa na viongozi, hakika kifo chake ni pigo kubwa’, ameongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa huo aliyefanya kazi kwa karibu na marehemu Munde,  Jackiline Kainja amekiri kuwa wamepoteza mtu muhimu sana, aliyejua siasa vizuri na aliyekuwa mstari wa mbele kuhakikisha CCM inapata ushindi mnono katika chaguzi zote.







Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.