NAIBU KATIBU MKUU CCM AONGOZA MAZISHI YA MNEC TABORA


Na Allan Kitwe, Tabora.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, John Mongella ameongoza umati wa wanaCCM na wakazi wa Tabora kumzika  aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mzee Nassoro Hamdan Seif.

Akitoa salamu za chama kwenye ibada ya mazishi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Mongella amemwelezea Mzee Hamdan kuwa ni Kiongozi aliyekitumikia chama kwa moyo wake wote hali iliyopelekea kuaminiwa na wanaCCM wote.

‘Ndugu zangu wana Tabora nachukua nafasi hii kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Dkt Asha-Rose Migiro kuwapa pole nyingi kwa kuondokewa na Mzee wetu, aliyekuwa Kada mwaminifu na nguzo muhimu ya Chama chetu’, ameeleza.

Mongella amebainisha kuwa enzi za uhai wake marehemu amefanya kazi kubwa ya kukiimarisha Chama na kukiwezesha kuibuka kidedea katika chaguzi za Urais, Ubunge na Udiwani na Serikali za Mitaa.

Ametoa wito kwa wanaCCM kuyaenzi mazuri yote aliyoyafanya alipokuwa Kiongozi katika nafasi mbalimbali na kuongeza kuwa umati mkubwa uliojitokeza kumsindikiza leo ni ishara ya matendo mema aliyowafanyia.

Enzi za uhai wake, Mzee Hamdan ameshika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Mshauri wa Chama, Naibu Meya wa Manispaa Tabora, Diwani wa Kata na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa.

Nyingine ni Mlezi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete na Mlezi wa Shule ya Watoto Wasioona ya Furaha iliyopo katika manispaa hiyo, pia alikuwa mdau mkubwa wa shughuli za maendeleo katika Mkoa huo na alijali sana watu.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Saidi Nkumba ameeleza kuwa marehemu ameacha pengo kubwa katika chama chao kwa kuwa alikitumikia kwa moyo wa dhati tangu akiwa kijana na kukiwezesha kupata mafanikio makubwa sana.

‘Mzee Hamdan amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha shughuli zote za chama zinafanikiwa na alijitoa sana kwa wana Tabora wote pasipo kujali itikadi za vyama vyao wala dini, hakika tutamkumbuka sana Mzee wetu’, alisema.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.