MWILI ULIOKATIKA VIPANDE WAKUTWA KWENYE RELI, TABORA

 


Na Allan Kitwe, Tabora.

MWILI wa mwanaume ambaye hajafahamika jina lake umekutwa kwenye reli ya treni huku ukiwa umekatwa vipande katika Mtaa wa Kombomasai, Kata ya Malolo, Manispaa ya Tabora huku ikihisiwa kuwa umeburuzwa na treni iliyopita usiku.

Akizungumzia tukio hilo jana diwani wa Kata hiyo Naomi Kasanga ameeleza kuwa akiwa nyumbani kwake saa 2 asubuhi alipigiwa simu na wananchi wakimjulisha kuwepo mwili huo kwenye reli ya treni ukiwa umekatika vipande.

Ameeleza kuwa alipofika eneo la tukio alikuta mwili huo wa mwanaume ambao unadhaniwa kuwa umeburuzwa na treni iliyopita usiku wa kuamkia jana baada ya kugongwa ila haijafahamika ni nani na alikuwa anatokea wapi.

‘Baada ya kuona mwili huo nilitoa taarifa kituo cha polisi na askari walikuja mara moja eneo hilo na kuuchukua kwa ajili ya uchunguzi zaidi, nashukuru sana wananchi kwa ushirikiano wenu na kunipa taarifa mapema’, amesema.

Mheshimiwa diwani ameomba Wataalamu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuweka alama ya hatari katika eneo hilo la makutano ya reli na barabara ya Tabora-Kigoma kwa kuwa eneo hilo limekuwa na matukio mengi ya ajali ya treni.

Ameongeza kuwa eneo hilo zinapita treni za kutoka Kigoma na Katavi, lakini hakuna tahadhari yoyote inayochukuliwa na Shirika pindi treni inapokaribia kupita, jambo ambalo ni hatari sana, hata honi siku hizi treni hazipigi.

Mkazi wa Mtaa huo Moses Johari amesema kuwa eneo hilo ni hatarishi ndio maana ajali za treni zimekuwa zikitokea mara kwa mara na kusababisha madhara makubwa kwa vyombo vya moto na binadamu kupoteza maisha.

‘Tunaomba serikali kupitia Shirika la Reli wachukue hatua za haraka kujenga kizuizi eneo hilo ili kuepusha ajali za mara kwa mara, hapa kuna uzembe kwa wataalamu wetu, mbona zamani ajali zilikuwa hazitokei’, ameshauri.

Ofisa Mnadhimu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora Omari Simba amefafanua kuwa kulingana na mazingira ya mwili huo ni wazi kuwa marehemu atakuwa amegongwa na treni na kuburuzwa kwenye reli hiyo.

Amedokeza kuwa tayari wamepeleka mwili huo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete, kwa ajili ya uchunguzi zaidi, taratibu zingine zitafuata.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.