JIMMY LAI AFUNGWA MIAKA 20 JELA KWA KUUNGA DEMOKRASIA.

 


Hong Kong - China.

MAHAKAMA ya Hong Kong imemhukumu bilionea anayefahamika kwa kuunga mkono demokrasia, Jimmy Lai, kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya ukiukaji wa usalama wa taifa mwezi Desemba.

Hukumu hiyo ndiyo kali zaidi kuwahi kutolewa chini ya sheria tata ya usalama wa taifa, ambayo China inadai ni muhimu kwa uthabiti wa jiji hilo.

Lai, mwenye pasipoti ya Uingereza, alikuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa Beijing, akitumia mara kwa mara gazeti lake la kidemokrasia Apple Daily kama chombo cha kupinga utawala huo.

Wakuu sita wa zamani wa gazeti hilo pia wamehukumiwa kifungo cha jela siku ya Jumatatu, kati ya miaka sita na miezi tisa hadi miaka 10.

Kwa wanaharakati wa demokrasia, Lai anaonekana kama shujaa, lakini kwa Beijing anachukuliwa kuwa msaliti.

Amekuwa akikanusha mashtaka yote dhidi yake, akisema alitetea kile alichoamini kuwa ni maadili ya Hong Kong, ikiwemo utawala wa sheria na uhuru wa kujieleza.

Hukumu hiyo ina maana kuwa huenda akawa na umri wa miaka 96 atakapoachiliwa huru mwaka 2044.

Serikali ya Taiwan imeitaka China na Hong Kong kusitisha mara moja mateso ya kisiasa na kumuachilia Lai.

Binti yake, Claire Lai, ameieleza hukumu hiyo kuwa ya “kikatili na ya kuvunja moyo,” akiongeza kuwa afya ya baba yake imezorota katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

“Atakufa shahidi akiwa gerezani,” amesema.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.