CCM: MAKAMPUNI YASIYOLIPA WAKULIMA YAPIGWE ‘STOP’
Na Allan Kitwe, Tabora
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Bodi ya Tumbaku (TTB) nchini kuchukua hatua mara moja dhidi ya Makampuni yote yanayonunua zao la tumbaku na kushindwa kulipa wakulima kwa wakati, na kushauri wapigwe stop.
Ushauri huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Komredi Saidi Nkumba alipokuwa akitoa salamu za chama katika Mkutano Mkuu wa 33 wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku (WETCU) Mkoani Tabora.
Amesema kuwa haingiii akilini kuona mkulima akihangaika kuandaa shamba lake mwaka mzima tena kwa gharama kubwa ili kuhakikisha anapata tumbaku nzuri inayokidhi viwango vya soko la ndani na nje lakini anapouza halipwi kwa wakati.
‘Chama Cha Mapinduzi hakifurahishwi na hali hii, Wanunuzi wote wanaokuja kununua mazao ya wakulima wanatambulika kisheria na wanapewa leseni, kama hawafanyi kile kinachotakiwa kuna haja gani ya kuwabembeleza’, ameeleza.
Komredi Nkumba ameitaka Bodi ya Tumbaku kusimamia ipasavyo zao hilo ili mkulima anufaike na jasho lake, aidha aliwataka kuweka utaratibu utakaowabana wanunuzi ili wasifanye kazi kwa mazoea na wanaponunua walipe kwa wakati.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Paul Chacha, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dk Gerald Mongela ameeleza kusikitishwa na utendaji wa Bodi ya Tumbaku (TTB) kwa kuwa imeshindwa kuwabana wanunuzi hali inayopelekea kulalamikiwa.
‘Kila mwaka tunakemea na kudhibiti vitendo vya utoroshwaji tumbaku ili isiuzwe kiholela na kuwakosesha wakulima mapato halali, lakini kama hawalipwi fedha zao kwa wakati tunawaonea, TTB mnatuchosha, badilikeni’, ameongeza.
Mheshimiwa DC ametumia mkutano huo kuagiza Makampuni yote ambayo hayajalipa fedha za wakulima za msimu uliopita kulipa mara moja vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kupigwa stop kabisa.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya WETCU Hassan Kitunga ameeleza kuwa Bodi hiyo imeaminiwa na wakulima kusimamia shughuli zao ili kilimo hicho kilete tija katika maisha yao na changamoto zilizopo zifanyiwe kazi mara moja.
Amebainisha kuwa bei ya tumbaku kwa msimu huu imeshuka kidogo kuliko msimu uliopita kutokana na kuporomoka kwa bei ya soko la dunia ila akawataka kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea na vikao vya majadiliano ili kuongeza bei hiyo.





Maoni