BINTI MCHOMA MAHINDI TABORA AWEZESHWA MTAJI WA LAKI 3
Na Allan Kitwe, Tabora.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka ameleta neema kwa kijana muuza mahindi ya kuchoma Hadija Seif (26) mkazi wa Kata ya Ng’ambo, Manispaa ya Tabora baada ya kumwezesha mtaji wa shilingi laki 3.
Waziri amemwezesha mtaji huo leo alipokuwa akifungua Jukwaa la Vijana wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati vilivyopo Mkoani Tabora, katika ukumbi wa Chuo Cha Utumishi wa Umma Mjini hapa.
Ameeleza kuwa jana akiwa katika pita pita yake mitaani baada ya kuwasili Mjini Tabora alimwona dada mmoja akichoma mahindi na alipomuuliza mradi huo unamsaidiaje akasema kuwa unampatia kipato kidogo cha kutunza watoto wake.
Na alipomuuliza ndoto yake ni nini, akaeleza kuwa anatamani kuwa na biashara ya kuuza vyombo vya nyumbani na kuuza samaki wa kukaanga, ila mtaji hana na alipoulizwa anatamani kuwa na mtaji wa kiasi gani akasema laki 3.
‘Sikujitambulisha kuwa mimi ni Waziri ila nilimwambia aje ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kuna mkutano wa vijana, nikampa namba, na leo amekuja, njoo uchukue ule mtaji (shilingi laki 3) ukaendeleze biashara yako’, amesema.
Akitoa shukrani zake Hadija ambaye mume wake alifariki, ameeleza kujawa na furaha isiyo kifani kwa kuwezeshwa kiasi hicho na mtu ambaye hakumfahamu, kumbe ni Waziri wa Vijana.
‘Nashukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa upendo wako wa hali ya juu na kujali maisha ya vijana, ambao hawana matumaini yoyote ya kuinuka kiuchumi, hakika umenifuta machozi, Mwenyezi Mungu akubariki sana’, ameeleza.
Akifafanua zaidi Hadija ameeleza kuwa kiasi hicho kitamsaidia kuongeza mtaji wa kuchoma mahindi na kuanzisha biashara nyingine ya kukaanga samaki, kwani awali alikuwa na mtaji wa shilingi 10 akaanzisha biashara ya kuchoma mahindi.
Katika mkutano huo Mheshimiwa Waziri amewataka vijana wote kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotangazwa na serikali ya Awamu ya Sita ili kuwezeshwa mikopo nafuu isiyo na riba ili kujikwamua kiuchumi.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha shilingi bilioni 200 kuwezeshavikundi mbalimbali vya vijana mikopo nafuu ili kuanzisha miradi yao pasipo kikwazo chochote.





Maoni