WAZIRI MKUU KUZINDUA MELI YA MV NEW MWANZA KESHO
Na Mwandishi Wetu, Mwanza.
MELI ya MV.New Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 kwa pamoja katika Ziwa Victoria inatarajiwa kuzinduliwa kesho Januari 23, 2025 mkoani Mwanza huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.
Akizungumza leo na waandishi wa habari mkoani Mwanza, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema mpaka kukamilika kwa ujenzi wa meli hiyo zaidi ya Bilioni 120 zimetumika huku katika uongozi wa Serikali ya awamu ya sita zaidi ya Bilioni 79 zikitolewa.
"Ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, pamoja na magari makubwa 3 na magari madogo 20. Meli hii imeundwa kwa viwango vya kimataifa na ina urefu wa mita 92.6, karibu sawa na uwanja wa mpira wa miguu, na upana wa mita 17, ikiwa na kimo cha ghorofa nne," amesema.
Profesa Mbarawa amesema hadi sasa meli ya MV New Mwanza tayari imeshafanya jumla ya safari sita (6) kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo.
"Katika safari hizo, meli imebeba jumla ya abiria 7,028 na kusafirisha takribani tani 673 za mizigo, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo katika Ukanda wa Ziwa Victoria.
Hata hivyo Profesa Mbarawa amesema kabla ya uzinduzi huo, Dk Mwigulu Nchemba atafanya ziara ya kikazi katika Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Kuratibu Shughuli za Utafutaji na Uokoaji (MLVMCT) kilichopo Wilaya ya Ilemela eneo la Uwanja wa ndege Mkoani Mwanza.
"Lengo la ziara hiyo ni kukagua na kujionea hatua ya ujenzi wa Kituo hicho ikiwa ni pamoja na maandalizi, mifumo ya uratibu, na kuona uwezo wa kitaalamu uliopo katika kukabiliana na matukio ya dharura yanayohusisha utafutaji na uokoaji, hususan katika maeneo ya Ziwa Victoria na maeneo jirani na namna kitakavyofanya kazi," amesema.

Maoni