MWENYEKITI BODI YA NRH AZINDUA RASMI SHUGHULI ZA UJENZI JENGO LA GHOROFA IDARA YA MATERNITY.














Na Mwandishi Wetu, Igunga.

MWENYEKITI wa bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Nkinga (NRH) iliyopo Kata ya Nkinga Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, Askofu Sixberth Kuzenza wiki hii amezindua rasmi shughuli za ujenzi wa jengo jipya lenye ghorofa katika Idara ya mama na mtoto zinazotazamiwa kuanza mapema mwaka huu 2026.

Tukio hilo la kihistoria limefanyika kwa ishara ya kuchimba udongo katika eneo ambalo litajengwa jengo hilo, ambapo hivi karibuni shughuli za ubomoaji wa majengo yanayotumika zitaanza rasmi baada ya huduma zitolewazo mahali hapo kuhamishiwa eneo lingine.

Askofu Kuzenza amesema; wanamshukuru Mungu kwakuwa hatua hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango mkakati wa Hospitali wa miaka 5 kuhakikisha huduma na miundombinu ya taasisi inaboreshwa zaidi ili kuwapatia wananchi huduma katika mazingira bora.

"Tunamshukuru Mungu sana kwakuwa ni jambo lililokuwa kwenye mpango mkakati wa Hospitali, na sasa tunaanza kuona utekelezaji wake, tunamwamini Mungu litakamilika kwa wakati ili liweze kuwafaa akina mama" amesema Askofu Kuzenza.

Ameongeza, "Tumejiwekea malengo Hospitali yetu kuipandisha hadhi kutoka kuwa Hospitali ya Rufaa ngazi ya mkoa na kuwa ya Rufaa ngazi ya Kanda" amenukuliwa Askofu Kuzenza.

Mwakilishi wa bodi ya Nkinga Friends toka nchini Sweden ndg.Mattias Lägermo amesema, amejisikia vizuri kuwa Nkinga wakati historia mpya inaenda kuandikwa, na kubainisha kwamba hadi mwisho wa mwaka huu sehemu ya jengo hilo itakuwa imesimama.

Dkt.Tito Chaula ni Mganga Mfawidhi amesema, jengo linalotumika sasa lilijengwa mwaka 1948 hivyo limekuwa halikidhi mahitaji ya sasa, kwani halina huduma za mtoto karibu kama vile Premature UNIT na NICU.

Amesema, huduma za mtoto kwa miaka mingi zimekuwa zikipatikana umbali mrefu takribani mita 700 toka anapolqzwa mzazi, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa mzazi anapohitaji kumuhudumia mtoto au kama amejifungua kwa njia ya Upasuaji.

Jengo jipya la ghorofa linalojengwa litakuwa na huduma zote muhimu za mama na mtoto ikiwemo, kitengo cha NICU, Premature, Vyumba vya kisasa vya kujifungulia, Wodi za kisasa, HDU ya kisasa, Theatre ya Mama mzazi na huduma zingine muhimu.





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.