MSTAHIKI MEYA AWANYOSHEA KIDOLE WASIOENDELEZA VIWANJA
Na Allan Kitwe, Tabora.
MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora Ghullam Hussein Dewj amewataka wananchi wote wenye viwanja katika maeneo mbalimbali ndani ya manispaa hiyo kuviendeleza ili Mji huo uonekane vizuri zaidi.
Ametoa rai hiyo alipokuwa akiongea na Wataalamu, Watendaji na Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kwenye kikao cha madiwani ambako alielekeza wahusika wote kuandikiwa barua ya kukumbushwa kuendeleza maeneo yao.
Amedokeza kuwa manispaa hiyo inakua kwa kasi kubwa sana kutokana na kazi nzuri ya utekelezaji miradi ya maendeleo inayoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
‘Mji wetu umeendelea kuboreshwa zaidi, lakini baadhi ya maeneo kuna viwanja havijaendelezwa, hali inayosababisha maji kutuama na kusababisha mafuriko, tunataka viwanja vyote viendelezwe, wahusika wakumbushwe’, ameagiza.
Aidha Mstahiki Meya amewataka kufuatilia maeneo yote ambayo hayajapangwa vizuri ili utaratibu wa kuyafanyia marekebisho ufanyike ili Mji uwe katika mpangilio mzuri.
Ameongeza kuwa baadhi ya Mitaa vibanda vya biashara na mama lishe wanafanya shughuli zao kwenye eneo la barabara hivyo kukosekana eneo la kupitisha mitaro ya maji hali hii huleta usumbufu mkubwa kwa jamii na kuathiri barabara.
Kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo katika eneo lake, kero au changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza kwenye maeneo ya makazi ya watu zitamalizika na Mji utakuwa katika mpangilio mzuri.
Aidha Mstahiki Meya amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo Dkt John Pima kuhakikisha maeneo yote ya Mji huo yanapitika vizuri hasa katika kipindi hiki cha mvua ili watoto wasikwame kwenda shule.



Maoni