WAZIRI SHARIFF AZINDUA JENGO LA MRI HOSPITALI YA ABDULAA MZEE
Na Mwandishi Wetu, Pemba.
WAZIRI wa Kazi na Uwekezaji Shariff Ali Shariff amesema Uwepo wa huduma ya MRI katika Hospitali ya Abdulaa Mzee Mkoani, Pemba ni hatua kubwa katika kuimarisha uwezo wa mfumo wetu wa afya na utawezesha wagonjwa kupata uchunguzi wa haraka, sahihi na wa uhakika.
Hayo ameyaeleza katika Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani wakati wa alipofungua jengo la huduma za MRI ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za Miaka 62 ya Mapinduzi Zanzibar.
Waziri Shariff amesema huduma ya MRI itaongeza uwezo wa madaktari kufanya maamuzi ya kitabibu kwa ufanisi zaidi, sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya afya na itasaidia kupunguza kuchelewa kwa matibabu, kuokoa maisha na kupunguza gharama kwa familia na Serikali kwa ujumla.
Aidha amesema kuwa uwamuzi wa kuanzisha huduma ya MRI kisiwani Pemba unaonesha wazi dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kusogeza huduma muhimu karibu kwa wananchi na kupunguza rufaa zisizo za lazima, kuimarisha usawa wa upatikanaji wa huduma na kuimarisha ustawi wa jamii.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema mradi huo umejengwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mkandarasi Benchmark Engineering Company Ltd, na kusimamiwa na Wizara ya Afya na ujenzi wa jingo hilo umegharimu jumla ya shilingi za Tanzania 564,024,120 ambapo tayari kiasi cha shilingi 368,394,390.69 sawa na asilimia 65 zimeshalipwa.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo na kuanza rasmi kwa huduma za MRI kunatoa fursa kubwa ya kuimarisha kiwango cha utoaji wa huduma kisiwani Pemba na itapunguza kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa kwenda Unguja sambamba na kupunguza gharama kwa familia.
Dkt Mngereza amesema jengo hilo lina jumla ya vyumba vinne vilivyopangwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu vya utaoaji wa huduma za uchunguzi wa MRI, vyumba viwili vimewekewa mashine za MRI pamoja na vifaa vyake.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwasogezea wananchi huduma kwa ukaribu kuanzia mindombinu ya afya, vifaa tiba na huduma za Uchunguzi jambo ambalo linawarihisia wananchi kupata huduma bora





Maoni