WASIMAMIZI WA USAILI WAPEWA MAFUNZO MAALUM




Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam.

KATIBU wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Mick Kiliba ameongoza kikao kazi cha Mafunzo kwa wasimamizi wa usaili Mkoa wa Dar es Salaam jana tarehe 14 Desemba, 2025 katika Ukumbi wa Karimjee.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika kila mkoa Nchini yakiwa na lengo la kuwakumbusha wasimamizi wa usaili kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu za uendeshaji wa mchakato wa ajira ili kuhakikisha haki inatendeka na wasailiwa wanapata kazi kulingana na uwezo na umahiri waliouonyesha katika saili hizo.

“Mwanzoni mwa mwezi wa kumi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa ahadi ya kuajiri nafasi 12,000 za kazi ndani ya siku 100 za kwanza baada ya kuapishwa, ambapo nafasi 5000 ni kwa kada za Afya na nafasi 7000 kwa kada za Elimu.

 Sekretarieti ya Ajira ilishaanza kazi ya kutekeleza Maagizo hayo na leo hii nyinyi mmeteuliwa kuhakikisha adhma ya Mhe. Rais inatekelezwa kwa wakati ili kabla ya siku 100 kufika tuwe tumekamilisha kupata wataalamu wenye sifa na weledi, Hivyo ninawaomba mkawatendee Haki Watanzania, msimpendelee wala kumuonea mtu, Hakikisheni Serikali inapata wataalamu bora kuingia katika Utumishi wa Umma.” Alisema Kiliba

Aidha, Kikao hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, chini ya Katibu Tawala wa Mkoa huo ambapo Ndg. Laurence Malangwa Katibu Tawala Msaidizi, sehemu ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kwa niaba ya Katibu Tawala alituma Salamu za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiwataka watumishi walioaminiwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa kwa kuzingatia kanuni, sheria, na taratibu katika Utumishi wa Umma, kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa letu ili kukamilisha ahadi ya Mhe. Rais kwa Watanzania.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na watumishi wa umma kutoka Ofisi mbalimbali za Umma ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam ambao wameteuliwa kushiriki katika mchakato wa Ajira.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.