SOMO LA LEO KUTOKA RSA TANZANIA




KWAmujibu wa kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Kanuni za LATRA za Usajili na Uthibitishaji Madereva na Wahudumu wa Mabasi (THE LAND TRANSPORT REGULATORY AUTHORITY (CERTIFICATION OF COMMERCIAL VEHICLE DRIVERS AND REGISTRATION OF CREW) REGULATIONS)) 2020, Dereva aliyesajiliwa na Kuthibitishwa na LATRA ana wajibu ufuatao kama sehemu ya masharti ya Kuthibitishwa kwake: 

1. Kuzingatia mwendo kikomo (speed limits) uliowekwa barabarani kwa mujibu wa sheria;

2. Kutoendesha gari huku akiwa amelewa pombe au madawa ya kulevya;

3. Kuheshimu amri halali ya askari polisi au maafisa wa LATRA;

4. Kuendesha gari akiwa na leseni hai na cheti cha uthibitishwaji

Kwa dereva anayeendesha gari la abiria, anatakiwa kuzingatia masharti yafuatayo ya ziada, kwa mujibu wa kanuni ya 10(2) ya kanuni tajwa hapo juu: 


1. Kutopakia abiria Zaidi ya uwezo wa gari kama ulivyoandikwa kwenye cheti cha usajili wa/au leseni ya, gari;

2. Kuhakikisha milango imefungwa kabla ya kuondoa gari;

3. Kuhakikisha gari lake lina leseni na bima hai;

4. Kuhakikisha anawataarifu abiria kuhusu mahitaji ya kiusalama ya gari lake, kabla ya kuanza safari. Mahitaji haya ni kama vile ulipo mlango au milango ya dharula, ilipo mitungi ya kuzimia moto, ikitokea dharula abiria wafanyaje, nk;

5. Kuwafikisha abiria mwisho wa safari yao kwa mujibu wa tiketi zao.

6. Kusimama katika maeneo ambayo kuna choo na huduma nyingine za kiutu;

7. Kuwa na batli (log book) na ratiba ya gari husika;

8. Kutoendesha gari kwenye ruti isiyo ya gari hilo;

9. Kutokatisha safari kabla ya kufika mwisho wa safari;

10. Kuvaa sare safi na nadhifu;

11. Kutojaza mafuta huku abiria wakiwa ndani;

12. Kuhakikisha kuwa burudani inayotolewa ndani ya gari lake inaendana na maadili na tamaduni za kitanzania, na kwa sauti isiyo ya juu;

13. Kuhakikisha hakuna mtu anayefanya biashara ndani ya gari, kuhubiri, kufanya shughuli za kisiasa, au kuonesha Sanaa au burudani ndani ya basi;

14. Kutowanyanyapaa au kuwaonea abiria au watumiaji wengine wa barabara;

15. Kutoshawishi au kujihusisha na harakati zozote zenye lengo la kusimamisha utoaji wa huduma ya usafirishaji abiria;

16. Kwa mabasi ya masafa marefu, kuhakikisha mfumo wa ufuatiliaji mwendo (VTS) unafanya kazi, kutouharibu mfumo huo, na ahakikishe anatumia kitufe cha utambuzi  wa dereva (driver identification key) 

*JE, DEREVA WA BASI LA ABIRIA UNAZINGATIA HAYA?*

Je, unajua madhara ya kutozingatia masharti tajwa hapo juu? Kwa taarifa yako, ukiukwaji wa masharti tajwa hapo juu unaweza kupelekea kufungiwa kuendesha gari au kunyang’anywa cheti cha thibitishwaji ambapo hutakaa uendeshe gari yoyote yenye leseni ya LATRA. Iwapo mamlaka itaamua kukutoza faini, basi faini yake ni isiyopungua shilingi 50,000 na isiyozidi shilingi 100,000. Madhara mengine ya kukiuka masharti ni kupoteza point kwenye leseni ya usafirishaji.


RSAadmin1

RSA Tanzania

USALAMA BARABARANI NI JUKUMU LETU SOTE.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.