MAGE NELSON MWENYEKITI MPYA TAWOMA MIRERANI

 




Na Mwandishi wetu, Mirerani 

MFANYABIASHARA maarufu wa kuongeza thamani madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Magreth Nelson amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama cha wanawake wanaojihusisha na shughuli za madini Tanzania (TAWOMA) Tawi la Mirerani.

Mage atatumikia kwa muda wa miaka mitano nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa wanawake wafanyabiashara wa magonga ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani.

Katika uchaguzi huo uliofanyika chini ya Makamu Mwenyekiti wa TAWOMA, Rachel Joseph Njau na Katibu Mkuu wa TAWOMA, Salma Ernest Kundi na kusimamiwa na Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Komolo Swalehe Abdalah na mjumbe wa MAREMA Tawi la Mirerani Jafar Matimbwa na kushuhudiwa na Afisa maendeleo ya jamii mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani Floriana Mcharo.

Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Komolo, Swalehe Abdalah akitangaza matokeo hayo amesema Magreth Nelson ambaye hakuwa na mpinzani alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 95.

Amesema Pendo Malifedha alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kura 93 na Chausiku Marwa alichaguliwa kuwa Katibu TAWOMA kwa kura 91.

Ameeleza kwamba nafasi ya Katibu msaidizi imeshikwa na Siana Mmasy aliyepata kura 69 dhidi ya Teddy Clement aliyepata kura 26.

Amesema Mweka hazina wa TAWOMA Tawi la Mirerani amechaguliwa Veronica Mwita kwa kura 93 na Mweka hazina msaidizi ni Khadija Ally aliyepata kura 92.

Amewataja wajumbe watano wa TAWOMA Tawi la Mirerani ni Mary Mnyawi, Mary Mdee, Halima Maganga, Adelfina Mboya na Zubeda Iddy.

Mwenyekiti mpya wa TAWOMA Tawi la Mirerani, Magreth Nelson amewashukuru wanawake hao kwa kumpa imani kubwa na kumchagua kwa kura zote kuwa kiongozi wao hivyo atawatumikia kwa moyo mmoja.

Mage amewapongeza wanawake 21 waliokata leseni kwa kila mmoja hivyo waendeleze umoja na mshikamano ili waliobaki nao wapate leseni ya kila mmoja wao.

Amewaahidi utumishi mwema na uliotukuka kwa kipindi chote atakachokuwa Mwenyekiti wao hivyo wampe ushirikiano wa kutosha katika kutumikia nafasi hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa TAWOMA Taifa Rachel Njau ambaye pia ni Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani amewasihi wanawake hao waongeza thamani madini ya Tanzanite kupendana, kushirikisha na kuondokana na maneno uzushi au masengenyo.

"Tuleni keki iliyopo hapa Mirerani na tuachaneni na kelele zisizo na maana yoyote ile na vitisho kuwa kuna watu watafutiwa leseni ili hali wamepatiwa kihalali," amesema Rachel.

Diwani wa Kata ya Mirerani, Salome Mnyawi, ambaye ni mlezi wa kikundi hicho amewapongeza viongozi hao kwa kuchaguliwa na kuwaasa waendelee kutumikia jamii inayowazunguka.

"TAWOMA Tawi la Mirerani, imefanya mambo makubwa ikiwemo kujenga maabara ya shule ya sekondari Tanzanite na kununua nguo na viatu vya watoto yatima na kutoa mahindi kwa msaada wa maafa ya Hanang' na vitongoji vya mji mdogo wa Mirerani," amesema Salome.

Afisa maendeleo ya jamii mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Floriana Mcharo amewapongeza viongozi hao na kuwaasa wachambgamkie fursa zilizopo serikalini kupitia vikundi.

Floriana amesema hivi sasa kila halmashauri ya mji, wilaya na manispaa, kupitia Serikali kuu wameweka utaratibu wa kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani, isiyo na riba ya riba, kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hivyo wanawake hao wachangamkie fursa hiyo.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.