KALEYA MOLLEL ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI MPYA SIMANJIRO
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI wa Kata ya Msitu wa Tembo, Kaleya Melita Mollel amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, kwa kura zote 24 za Madiwani waliohudhuria kikao.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa wilaya ya Simanjiro, Edosi Evaristi Ndikwiki amesema Mollel ambaye ni Diwani wa Kata ya Msitu wa Tembo, amepata kura zote 24 zilizopigwa
Ndikwiki pia amesema, madiwani hao wamemchagua Diwani viti maalum wa Tarafa ya Terrat, Mwanjaa Jacob kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kura zote 24 za ndiyo.
Amesema katika uchaguzi huo uliofanyika mji mdogo wa Orkesumet ulihusisha madiwani wote wanaotokana na CCM wa kata zote 18 na viti maalumu sita.
Ndikwiki amewaasa madiwani hao kutoa ushirikiano kwa wataalam wa halmashauri hiyo kwani wameshaapa kutumikia nafasi zao.
"Tuzingatie mahusiano mazuri na watumishi, tuwape ushirikiano na tuwe watatuzi wa migogoro tusiibue migogoro ambayo itaturudisha nyuma na kutuondoa katika lengo letu la kusuka mbele gurudumu la maendeleo," amesema.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Jackson Kisaka amesema Diwani ni mwakilishi wa wananchi hivyo wasiende kuzua migogoro bali kutatua migogoro hasa ya ardhi.
"Leo mmekula kiapo mnapaswa kutambua kuwa ninyi ni viongozi ukiwa Mwenyekiti wa maendeleo wa kata unapaswa kutambua wajibu wako katika kutumikia nafasi hiyo ya uongozi," amesema Kisaka.
Mwenyekiti mpya wa halmashauri ya wilaya hiyo Kaleya Melita Mollel amewashukuru madiwani hao kwa kumpa kura zote za ndiyo 24.
"Naombeni ushirikiano kwani wote tunajifunza twendeni tukawatumikie wananchi waliotuchagua na kutatua kero zao kwa lengo la kufanikisha maendeleo," amesema Mollel.
Mwenyekiti Mollel amewataja wajumbe wa kamati ya fedha, uongozi na mipango ni Makamu Mwenyekiti Mwanjaa, Albert Msole, Taiko Kurian Laizer, Jackson Ole Materi na Rehema Laizer.
Amesema Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Laizer amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya jamii ya elimu, afya na maji.
Amesema Diwani wa kata ya Ngorika Albert Msole amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira.
Amewataja wajumbe wa kamati ya ardhi ni Diwani wa kata ya Mirerani Salome Mnyawi na Diwani wa kata ya Terrat, Jackson Ole Materi.
Wajumbe wa kamati ya ALAT Mkoa wa Manyara ni Diwani wa Kata ya Emboreet, Yohana Shinini na Diwani wa viti maalum Tarafa ya Moipo, Paulina Makeseni.

Maoni