ZAINABU AFANYA KAMPENI MLANGO KWA MLANGO KUSAKA KURA ZA UBUNGE JIMBO LA KIVULE.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
MGOBEA Ubunge Jimbo la Kivule, Ilala, Dar es salaam, kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Bi. Zainabu Ham Abdul, ameahidi kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuwatumikia Wananchi, atahakikisha anaboresha huduma mbalimbali za kijamii katika jimbo hilo akiangazia utoaji wa fursa kwa watu wenye ulemavu na makundi maalum, huduma bora za afya, elimu, upatikanaji wa maji safi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
Bi. Zainabu anaefanya kampeni zake mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba, kijiwe kwa kijiwe amesema kuwa, iwapo atapewa dhamana ya kuliongoza jimbo hilo, pamoja na mambo mengne atahakikisha anashirikisha jamii kupitia fursa za kiuchumi kwa vijana, wanawake, ikiwemo kuwasemea watu wenye ulemavu ili kila mmoja aweze kunufaika na rasilimali zilizopo kwa usawa na uwazi.
Naye Meneja wa Kampeni wa mgombea huyo, Bw. Komein Rwihula, amewaomba wananchi kumchagua mgombea wao, ili akafungue ukurasa mpya wa maendeleo kwa wananchi wa Jimbo la Kivule na kusisitiza umuhimu wa kuwapa fursa watu wenye ulemavu, na makundi maalumu kwani kufanya hivyo ushiriki wao utasaidia katika utoaji wa maamuzi kwa maendeleo ya taifa la Tanzania.
Wananchi waliotembelewa na Mgombea huyo wameeleza kuvutiwa na sera zake zinazoashiria kuwa anaweza kuwatumikia endapo watampa nafasi.

Maoni