WANAFUNZI WATAKIWA KUDUMISHA AMANI NA MSHIKAMANO




Na Mwandishi Wetu, Mara.

AFISA Ushirikishwaji Jamii Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Thomas Mapuli, Oktoba 22,2025 amekutana na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mshikamano iliyopo katika Manispaa ya Musoma, ambapo ametoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kutunza amani katika jamii.

Akizungumza na wanafunzi hao shuleni hapo ACP Mapuli aliwasisitiza vijana kuwa mabalozi wa amani na kuzingatia maadili mema, huku akiwataka kujiepusha na vitendo vya vurugu, ubaguzi, na ukatili wa aina yoyote, ikiwemo ule wa kijinsia.

Aidha, aliwahimiza wanafunzi kuzingatia masomo yao na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuhatarisha ndoto zao za baadaye, akibainisha kuwa elimu ndiyo ngao kuu ya kupambana na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

“Jamii yenye amani huanza na mtu mmoja mmoja. Ninyi kama vijana mna wajibu wa kuwa mfano wa kuigwa, kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya ukatili wa kijinsia, na kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa za vitendo hivyo pindi vinapotokea,” alisema ACP Mapuli.

Wanafunzi na walimu wa shule hiyo wamelipongeza Jeshi la Polisi mkoa wa Mara kwa kuendelea kutoa elimu ya ulinzi na usalama wa jamii mashuleni, wakisema hatua hiyo inasaidia kuongeza uelewa na kupunguza vitendo vya ukatili vinavyowakumba hasa watoto na vijana.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.