VIONGOZI WA DINI WAKEMEA WANAOTAKA KUANDAMANA




Na Allan Kitwe, Tabora.

VIONGOZI wa madhehebu ya dini kutoka Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi wameiasa jamii kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu amani ikiwemo kushiriki maandamano yanayolenga kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

Wakiongea katika Kongamano Maalumu la Amani lililofanyika leo katika ukumbi wa Panasonic Mjini Tabora wameeleza kuwa maandamano na vurugu hayajengi bali yanabomoa misingi ya amani na kuongeza chuki na uhasama.

Akifungua Kongamano hilo Shehe wa Mkoa wa Tabora Ibrahimu Mavumbi ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Maridhiano ya Amani ya Mkoa amesema kuwa amani ni tunu muhimu sana kwa maendeleo ya taifa lolote lile.

Amesisistiza kuwa ni muhimu sana jamii ikaelimishwa umuhimu wa kudumisha amani na upendo na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29.

‘Watanzania tusikubali kuliingiza taifa kwenye machafuko, kipindi hiki tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ni kipindi muhimu sana, tunapaswa kuwa watulivu ili kupata viongozi bora’, amesema.

Shehe amebainisha kuwa hakuna dini inayoruhusu vurugu na machafuko, akadokeza kuwa kongamano hilo limekuja wakati mwafaka kwa kuwa halikubaliani na vitendo hivyo na linakemea wale wote wanaotaka kuandamana.

Wawezeshaji wa Kongamano hilo Shehe Ramadhan Khamis kutoka Mwanza na Askofu Denis Nkwera wa Kanisa la Pentekoste wameeleza kuwa vitabu vitakatifu vya korani na biblia vikataza mioyo iliyojaa roho ya machafuko.

Viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana ya kujenga jamii iliyo na hofu ya Mungu na kukemea waumini wao wanaojiingizii katika matukio yaliyo kinyume na mpango wa Mungu ambayo hayajengi bali kubomoa amani na utulivu wa nchi.

‘Mtu yeyote anayechochea vurugu au kufanya jambo lolote linalopelekea uvunjifu wa amani, anaenda kinyume na maandiko matakatifu na Mwenyezi Mungu hapendezwi naye hata kidogo’, amesema Askofu Denis.  

Mchungaji Edward Kadanga wa kanisa la SDA Urambo na Shehe Idd Suleiman wa Igunga wametoa wito kwa waumini wa dini zote kumrudia Mungu na kujiepusha na vurugu, matusi na maandamano bali waheshimu Mamlaka iliyopo madarakani.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.