TAKUKURU YAKABIDHI MSAADA WA VIFAA TIBA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA YA MBEYA.
Na Mwandishi Wetu,
KATIKA juhudi za kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongzwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maboresho makubwa yaliyofanyika kwenye sekta ya afya na kuimarishwa kwa huduma zinazotolewa kwa Wananchi, Watumishi wa Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) leo imekabidhi mashine mbili za kisasa za huduma ya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda, maarufu kama watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila alisema, “Hospitali zina mahitaji mengi na Serikali yetu inajukumu kubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora. Hivyo ni wajibu wa kila mwananchi mzalendo wa nchi hii kuchangia ili kuimarisha sekta ya afya na huduma nyingine muhimu.”
Chalamila amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa kuboresha huduma za afya nchini katika miundombinu, vifaa tiba, na watoa huduma.
"Watumishi wa TAKUKURU tumeona ni wajibu wetu kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa msaada huu wa mashine mbili za kisasa ambazo zitasaidia kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na uzito pungufu lengo ni kuhakikisha hospitali za rufaa za mikoa yote zinapata mashine kama hizo ili kuboresha huduma za kuokoa maisha ya watoto wachanga waliokwama kwa sababu ya ukosefu wa vifaa muhimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji amewashukuru watumishi hao wa TAKUKURU kwa msaada huo wa mashine za kisasa, akisema utaongeza nguvu katika huduma ya kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa mapema na kuwasaidia kuendelea kuishi na afya njema pia ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kwani mahitaji ya hospitali hiyo ni makubwa katika kutoa huduma.
Naye Mkuu wa Idara ya Watoto, Dkt. Nazareth Mbilinyi, amesema kuwa zaidi ya nusu ya watoto wanaozaliwa hospitalini hapo huzaliwa wakiwa na uzito pungufu au kabla ya muda wao, huku wengine wakikumbwa na changamoto ya ugonjwa wa manjano.
Ameongeza kuwa ujio wa mashine hizo ni faraja kubwa kwa timu ya madaktari na wauguzi wanaohudumia watoto hao kwani sasa watakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora zaidi kwa wakati muafaka.





Maoni