MGOMBEA UBUNGE KUPITIA CHAMA CHA WANANCHI (CUF) AUAWA KWA KUCHOMWA NA KITU CHENYE NCHA KALI
Na Mwandishi Wetu, Siha -Kilimanjaro.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Siha kupitia Chama cha Wananchi (CUF) mkoani Kilimanjaro, Daudi Wilbard Ntuyehabi, ameuawa na wananchi baada ya kudaiwa kumchoma kisu mtu mmoja aitwaye Abdul Issah Mohamed.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 7, 2025 katika Kijiji cha Kilingi, wilayani Siha.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, tukio hilo lilitokea majira ya saa 1:30 usiku, ambapo marehemu Daudi anadaiwa kumchoma kisu tumboni Abdul Issah Mohamed na kumsababishia utumbo kutoka Nike.
Inadaiwa kuwa Abdul alikuwa anajaribu kuingilia ugomvi uliokuwa ukiendelea kati ya Daudi na kijana mwingine waliokuwa wakizozana kuhusu deni la fedha wakiwa kwenye baa ya pombe maarufu kama ‘grocery’.
Baada ya tukio hilo, wananchi waliokuwepo eneo hilo walimshambulia Daudi hadi kusababisha kifo chake.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi linawashikilia watu nane kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi,Kamanda Maigwa ametaja majina ya wanaoshikiliwa kuwa ni Hamadi Issah Mohamed, Alphonce Kinyaha, Rizik Amedeus, Frank Paulo Lutindi, Shedrack Emanuel, Jeremia Mnkondo, Zainab Elisha na Issah Mohamed.
Ameongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea, huku akitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi, kwani imekuwa ikisababisha madhara makubwa katika jamii.
Kwa upande wake, Katibu wa CUF Wilaya ya Siha, Adamu Ramadhani, amesema kuwa chama hicho kimesikitishwa na tukio hilo na kitaendelea kutoa taarifa zaidi kadri muda unavyoenda na uchunguzi unavyoendelea.

Maoni