IGUWASA YATATUA KERO YA MAJI SHULE YA MSINGI CHIPUKIZI B IGUNGA.
Na Lubango Mleka, Igunga
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Igunga (IGUWASA) imefanikiwa kutatua tatizo sugu la maji katika Shule ya Msingi Chipukizi B iliyopo eneo la Mtaa wa Sanzura, Wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora.
Zaidi ya Wanafunzi 200 pamoja na Walimu na Wakazi wanaozunguka Shule hiyo wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama, hatua inayotarajiwa kusaidia kudhibiti milipuko ya magonjwa na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Wananchi waliozungumza na blogu ya Habari Kamili wakati wa zoezi la uchimbaji mtalo kwa ajili ya kulaza bomba la maji wamesema huduma hiyo ni faraja kubwa baada ya kusubiri kwa muda mrefu.
Maria Luhende, Rajabu Juma, Aisha Mussa, Elias Kishiwa na Paul Joseph, ni baadhi ya wakazi wa mtaa wa Sanzura waliojitokeza katika zoezi la uchimbaji wa mtalo wameipongeza IGUWASA kwa kufanikisha mradi huo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Stoo, Phabian Lushindika, amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa na amehamasisha wananchi kushiriki katika kulinda miundombinu ya maji ili idumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa IGUWASA, Alexander Ntonge, amesema mradi huo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa mteja ambapo mamlaka hiyo inatembelea maeneo mbalimbali yenye uhitaji wa huduma hiyo muhimu.















Maoni