WANANCHI RORYA WAHIMIZWA KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Na Mwandishi Wetu, Rorya Mara.
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu Ismail Ali Ussi amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Rorya kutumia nishati safi ya kupikia katika maeneo yao kutokana na faida mbalimbali zinazopatikana kwa kutumia nishati safi.
Akizungumza na wananchi katika Shule ya Sekondari Nyamunga, baada ya kutembelea mradi wa nishati safi wa shule hiyo, Ndugu Ussi amesema kwa kupikia nishati safi wananchi watapika kwa gharama nafuu na pia watakuwa wanatunza mazingira.
“Nishati safi inasaidia sana kwani gharama zake ni nafuu, haiathiri afya ya mtumiaji kama ilivyo katika matumizi ya kuni na mkaa na inasaidia kutunza mazingira yanayotuzunguka, hivyo ni muhimu sisi sote kutumia nishati safi majumbani mwetu” amesema Ndugu Ussi.
Ndugu Ussi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kwa kuwekeza fedha shilingi milioni 11 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo katika Shule ya Sekondari Nyamunga ambao amesema unalinda afya za wapishi na mazingira ya Halmashauri hiyo na kuwataka wananchi kuiga mfano huo kuboresha maisha yao.
Wakati huo huo, Mwenge wa Uhuru umeendelea na mbio zake katika Mkoa wa Mara ambapo leo tarehe 19 Agosti, 2025 umeingia katika Wilaya ya Rorya na kutembelea, kukagua, kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 2,531,470,759.63.
Fedha zilizogharimia miradi hiyo zimetokana na mchango wa wananchi shilingi 6,920,000; fedha za Halmashauri shilingi 184,876,550; Serikali Kuu shilingi 2,286,594,209.63 katika sekta za mazingira, huduma za kiuchumi, mifugo, elimu, maendeleo ya jamii, miundombinu na afya.
Mwenge umepokelewa katika Stendi ya Kinesi kutoka Wilaya ya Butiama na baadaye kuelekea Nyamunga Sekondari ambapo umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji Nyamunga na kukagua mradi wa nishati safi, kukagua klabu ya kuzuia na kupambana na rushwa katika Shule ya Sekondari Nyamunga.
Aidha, Mwenge wa Uhuru umetembelea skimu ya umwagiliaji ya Rabour, umeweka jiwe la msingi katika uzio wa mnada Nyamaguku, kuweka jiwe la msingi katika Sekondari ya Jafari Chege, kutembelea gereji ya pikipiki ya kikundi cha vijana wazalendo katika eneo la Utegi.
Katika Wilaya ya Rorya, Mwenge wa Uhuru umezindua daraja la mto Mabura na kalavati mbili za barabara ya Ryagoro-Saro, umeweka jiwe la msingi katika zahanati ya Randa na baadaye kuelekea katika mkesha katika uwanja wa Osogo eneo la Utegi.
Katika eneo la mkesha, Mwenge umepokea Risala ya Utii na kukagua halaiki, kupokea taarifa mbalimbali kuhusiana na maandalizi ya uchaguzi mkuu, masuala ya afya, lishe na kuzuia madawa ya kulevya na rushwa.
Kesho tarehe 20 Agosti, 2025 Mwenge wa Uhuru utaendelea na mbio zake katika Mkoa wa Mara ambapo utakimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime na mapokezi ya Mwenge yanatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Gamasara.






Maoni