WACHIMBAJI WADOGO 25 KATIKA MGODI WA NYANDOLWA WAMEFUKIWA NA KIFUSI.
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga.
JUMLA ya wachimbaji wadogo 25 katika mgodi mdogo wa Nyandolwa uliopo kijiji cha Mwongozo Halmashauri ya Shinyanga, wamefukiwa na kifusi baada ya mgodi kutitia.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wachimbaji katika eneo hilo wamefanya juhudi za kuwaokoa wachimbaji hao na tayari wachimbaji wawili wameokolewa.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amesema kuwa wachimbaji hao walikuwa katika mashimo matatu tofauti, ikiwemo shimo la duara namba 106 lenye watu 6, 103 lenye watu 11, na duara namba 20 lenye watu 8. Juhudi za uokoaji bado zinaendelea.
Tukio la kutitia kwa mgodi huo limetokea Agosti 11, 2025 saa nne asubuhi, wakati shughuli za matengenezo ya maduara hayo zikiendelea.
Mtatiro amewasihi wachimbaji kuwa watulivu wakati jitihada za kuokoa uhai wa walioko chini zikiendelea.

Maoni