MADEREVA, ABIRIA WAPATIWA ELIMU YA USALAMA BARABARANI NA MATUMIZI SAHIHI YA VYOMBO VYA KUZIMIA MOTO IGUNGA.
Na Mwandishi Wetu, Igunga.
MADEREVA na Abiria katika Kituo cha Mabasi Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora wamepatiwa Elimu ya Usalama Barabarani na Mabalozi wa Usalama Barabarani Wilaya ya Igunga (RSA) yenye lengo la kuendelea kuwakumbusha Madereva na Abiria kufuata sheria za usalama barabarani ili kunguza ajali zitokanazo na ubovu wa magari na uzembe wa Madereva.
Elimu hiyo imetolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la Road Safety Ambassadors (RSA) kwa kushirikiani na Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani na Jeshi la Zimamoto wilaya ya Igunga ambapo wametoa Elimu ya Usalama Barabarani, Wajibu na Haki za Abiria, Elimu ya tahadhari ya majanga ya Moto pia imbeambatana na zoezi la ukaguzi wa magari, vifaa vya kuzimia moto na ukaguzi wa leseni kwa madereva.
Akitoa Elimu ya tahadhari ya majanga ya moto Koplo Shadrack Mweya kutoka Jeshi la Zimamoto amewataka madereva kuhakikisha magari yao yanakuwa na vifaa vya kuzimia moto ambavyo havijaisha muda wa matumizi, milango ya dharura katika magari.
" Leo tupo hapa kituo cha mabasi Igunga tukiendelea kuwakumbusha madereva na abiria juu ya matumizi sahihi ya vyombo vya kuzimia moto na kukagua magari kama yana vifaa hivyo na madereva wanajua kuvitumia," amesema Koplo Mweya.
Huku Barozi wa Usalama Barabarani wilaya ya Igunga Faustine Saimon akibainisha lengo la ukaguzi wa magari na kutoa elimu hizo kwa abiria na madereva kuwa na kupunguza ajali zitikanazo na ubovu wa magari na uzembe unaofanywa na madereva na uendeshaji gari pasipo kufuata sheria za usalama barabarani.
Nao baadhi ya Madereva na Abiria wamelipongeza shirika la RSA, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto Igunga kwa kuendelea kuwakumbusha juu ya wajibu wa madereva na abiria wawapo safarini ili kuepuka ajali zitokanazo na uzembe wa madereva au abiria kwa kutokutoa taarifa pindi madereva wanapo vunja sheria.
"Kwa kweli leo nimefurahi kupata Elimu hii kwani ni jambo zuri sana kwetu madereva kukumbushwa kufuata sheria za usalama barabarani kwani wengi wetu wamekuwa wakiendesha magari kwa mazoea, wengine kufanya makusudi tu kuvunja sheria, leo tumeona baadhi ya madereva wakipigwa faini juu ya makosa kama kubeba abiria na mizigo mizito ndani ya gari," akisema Dereva Hussen Ally.
Huku Abiria Juma Abdalla akiomba zoezi hilo liwe endelevu kwa ukaguzi wa magari kabla ya kutoka kituoni na hata linapofika katika vituo vya ukaguzi wa magari, kwani litasaidia madereva na wamilikiki wa magari kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha mazoea, pia kutawafanya abiria wengi kujua haki na wajibu wao wawapo safarini kwani wengi hawajui haki zao.
Maoni