COOP BANK YAJIVUNIA UTOAJI HUDUMA SEKTA YA KILIMO.

. Coop Bank yatangaza Ushiriki Mkubwa katika Maonesho ya Nanenane,

Na Mwandishi Wetu, Dodoma. 

BENKI ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) imethibitisha kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Nanenane 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ikiwa ni miongoni mwa wa  dhamini wa maonesho hayo makubwa ya kilimo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la benki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank, Bw. Godfrey Ng’urah, amesema benki hiyo imejikita katika kutoa huduma za kifedha zenye kuleta mabadiliko chanya katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo-biashara, huku ikitoa kipaumbele kwa wakulima, vijana na wajasiriamali wa vijijini.

“Coop Bank ni benki ya ushirika kwa vitendo. Zaidi ya asilimia 51 ya umiliki wake upo mikononi mwa vyama vya ushirika hii ni benki ya wakulima, kwa wakulima,” amesema Bw. Ng’urah.

Ameeleza kuwa, Benki hiyo inashirikiana na vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vya ushirika (UNION) nchini kote katika kusaidia wakulima wa mazao ya kimkakati kama kahawa, chai, korosho, ufuta, mbegu za mafuta, pamba na mazao mengine yanayouzwa kupitia mifumo rasmi ya ushirika.






 “Tunatoa huduma za kifedha kwa ukusanyaji wa mazao, usindikaji, masoko na usafirishaji ndiyo maana tunashiriki Nanenane kwa nguvu; ni jukwaa letu la kukutana na wanachama wetu na wakulima wapya,” akiongeza kusema. 

Bw. Ng’urah pia amesema kuwa benki hiyo, iliyozinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Aprili 2025, tayari ina matawi katika mikoa ya Kilimanjaro, Tabora, Moshi, Mtwara na Dodoma, ikiwa na makao yake makuu jijini Dodoma.

Katika Maonesho ya Nanenane, Coop Bank imejipanga kutoa elimu na huduma za kifedha kupitia mabanda mawili banda la wadhamini wakuu na banda la Kijiji cha Ushirika ambapo wananchi, wakulima, vijana na wanawake wataweza kupata taarifa kuhusu mikopo, akiba, huduma za kidigitali na bidhaa nyingine za benki hiyo.

 “Tunawaalika wananchi wote kutembelea mabanda yetu na kujifunza zaidi kuhusu huduma zetu. Tumejipanga kuhakikisha wakulima wanakuwa na benki inayowajali na kuwasaidia kufanikisha ndoto zao,” akisema.





Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MWENYEKITI NAMALULU AWEKWA PEMBENI KUPISHA UCHUNGUZI

IGUNGA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NANENANE TABORA.